Submit Form Gallery Login/Ingia
National Investments Plc (NICOL)- Official Website
Submit Form Gallery Login/Ingia

TAARIFA KWA WANAHISA

Taarifa hii inahusu habari iliyosambaa katika vyombo vya habari hivi karibuni ambayo inabainisha kwamba Mheshimiwa Luhaga Mpina (MB), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alitengua Mkataba wa Mauzo wa Mali za Machinjio ya Dodoma (Dodoma abattoir) ulioingiwa kati ya Wizara na Kampuni ya Uwekezaji ya Taifa (NICOL), ikisemekana kwamba NICOL imeshindwa kutekeleza baadhi ya masharti ya Mkataba huo. Zaidi ya hapo, Waziri amenukuliwa kwamba aliamuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi ichukuwe mara moja mali zote za Kampuni ya Nyama, (Tanzania Meat Company Ltd. - TMCL) na vilevile akaagiza NICOL ilipe Wizara ya Mifugo na Uvuvi na TMCL jumla ya shilingi bilioni 15.

Kwa ufafanuzi, ieleweke kwamba mnamo mwaka 2008, baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuamua kusitisha uendeshaji wa shughuli za machinjio na kutangaza nia ya kuuza rasilimali za Dodoma Abattoir, ndipo tarehe 11 Septemba 2008, NICOL ilinunua mali hizo kwa kulipa Serikalini shilingi bilioni 1.3 fedha taslim, kiasi ambacho baadaye kilichukuliwa kama ni asilimia 51% ya mchango wa ubia kati yake na Serikali katika kampuni ya TMCL, na Serikali ilichukua asilimia 49% zilizobaki.

Kwa madhumuni ya kuepusha upotoshaji na kwa minajili ya kuzuia mkanganyiko wowote ambao unaweza kutokea kutokana na taarifa hizo, NICOL inapenda kufafanua kuwa ikiwa kama Mwanahisa, haikuhusika na wala haitakiwi, na haijawahi kamwe kuhusika na uendeshaji wa Tanzania Meat Company Ltd, ambayo ni kampuni huru iliyosajiliwa kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Cap. 212, tarehe 28 Julai, 2008; Namba ya Usajili 66751, na inasimamiwa na kuendeshwa na Menejimenti yake yenyewe ikiongozwa na Bodi ya Wakurugenzi inayoteuliwa na wanahisa wake; Wizara ya Mifugo na Uvuvi nayo huteua mjumbe mmoja katika Bodi hiyo. Kwa hivi sasa, TMCL ina wanahisa wawili; nao ni National Investments Plc (NICOL) ambayo inamiliki asilimia 51% ya hisa, na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), ikiwakilisha Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inayomiliki asilimia 49% ya hisa.

Kwa mujibu wa sheria, uendeshaji na uteuzi wa wafanyakazi wa kampuni yeyote unafanywa na Menejimenti ya kampuni husika ikiongozwa na Bodi ya Wakurugenzi. Wanahisa hawaruhusiwi katu kujihusisha na uendeshaji wa kampuni; jukumu la Wanahisa huishia katika kuweka na kusimamia sera. Kwa misingi hio, NICOL haijawahi kwa wakati wowote kusimamia uendeshwaji wa TMCL, zaidi ya kusaidia kutoa msaada wa kifedha, ambapo mpaka tarehe 30 Desemba 2019, zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zimetolewa kama mkopo nafuu bila riba, ili kukabiliana na madeni hatarishi, kulipia mishahara, madeni ya kodi za serikali, malipo mengine ya kisheria na ununuzi wa mitambo na ukarabati wa mashine. Hivyo basi, habari iliyosambazwa ikidai kuwa NICOL ilikuwa inaendesha Tanzania Meat Company Ltd sio sahihi, inapotosha na haikubaliki kisheria. Laiti kama utaratibu huo ungekuwa unatumika, angalau basi pangalikua na Mkataba wa Huduma za Uendeshaji (Management Service Agreement), ukieleza majukumu, masharti ya wahusika na ada.

Aidha, taarifa hizo zilidai pia kwamba NICOL ilikiuka vifungu kadhaa vya Mkataba wa Mauzo wa Mali za Machinjio ya Dodoma, jambo ambalo linasemekana lilipelekea Mheshimiwa Waziri aamuru kutenguliwa mara moja Mkataba wa Mauzo, na kutoa maagizo hatua kadhaa zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na kuweka shughuli zote za uendeshaji wa TMCL chini ya Wizara na kuteua Kaimu Meneja Mkuu kuiendesha kampuni. Katika mchakato huo, pia yalitolewa madai kadhaa dhidi ya NICOL ambayo hayakuthibitishwa, ikiwemo matumizi ya kibadhirifu ya fedha. Wanahisa wazingatie kwamba Mkataba wa Mauzo uliotajwa na Mheshimiwa Waziri ulikoma mara baada ya kuanzishwa na kusajiliwa kwa TMCL mwaka 2008, na kupewa umiliki wa mali zote zilizoainishwa katika mkataba huo kama sehemu ya rasilimali za kampuni. Hivyo basi, si NARCO wala NICOL inaweza kudai kwamba ina maslahi ya moja kwa moja katika umiliki wa mali za yaliyokuwa Machinjio ya Dodoma.

Wanahisa watakumbuka kuwa mnamo mwaka 2012, Mkutano Mkuu wa Wanahisa ulifukuza kutoka madarakani Bodi ya zamani ya NICOL kwa kushindwa kufuata miongozo ya Mamlaka za Udhibiti, misingi ya utawala bora na Sheria ya Makampuni. Changamoto hizo za uongozi mbovu wa Bodi ya NICOL ya wakati ule vilevile ziliathiri utendaji kampuni zake tanzu zote, ikiwa pamoja na shughuli za Bodi ya TMCL, ambayo ilidhoofika zaidi kutokana na king’ang’anizi cha Bodi ya NARCO kuendelea kutambua, kukumbatia, kuwatetea na kufanya kazi katika Bodi ya TMCL, kwa takriban miaka sita (6), na wakurugenzi waliokuwa wamefukuzwa na Wanahisa wa NICOL. Ni dhahiri kwamba katika kipindi chote hicho hakukuwa na ufanisi wala maendeleo chanya yoyote ya kibiashara kwa kuwa ufujaji mali na ubadhilifu ulitamalaki TMCL.

Mara baada ya kuteuliwa mwaka 2012, Bodi mpya ya NICOL iliomba mbia mwenza, NARCO, kushiriki katika jitihada za kuunda Bodi halali ya Wakurugenzi wa TMCL. NARCO walipinga na kukataa kutoa ushirikiano stahiki kwa kisingizio cha uwepo wa walichoita “migogoro ya ndani ya NICOL”. Msimamo huu vilevile baadaye uliungwa mkono na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Mheshimiwa Waziri aliyekuwepo wakati huo kabla ya uchaguzi mkuu 2015.

Ni muhimu sana kutambua kwamba tuhuma zote zilizotolewa dhidi ya NICOL katika taarifa inayodaiwa kutolewa na Mheshimiwa Waziri Mpina (MB) zinahusu matukio ya kipindi cha kati ya mwaka 2008 – 2016, na ni matokeo ya utendaji kazi duni na usimamizi mbaya wa Bodi ya TMCL ya kipindi hicho, ambayo haikuwa halali kwani ilijumuisha wakurugenzi waliofukuzwa na Wanahisa wa NICOL wakishirikiana na Bodi ya NARCO, kwa baraka za Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Bodi halali ya TMCL ilipoanza kazi mwaka 2016, ilichukua hatua za kinidhamu na vilevile kuchunguza ubadhirifu, na taarifa zilitolewa Wizarani na Polisi ambao walifungua Jalada la Uchunguzi wa Jinai Na. DOM/IR/5333/2017 baina ya TMCL na Leo Blasi Akonaay, na uchunguzi bado unaendelea, kama inavyodhihirishwa na mawasiliano kati ya wahusika Kumb DOM/CID/B.1/7/VOL.XL1/322 ya tarehe 27 Desemba 2018.

Aidha, kiutendaji Bodi halali ya TMCL vilevile ilichukua hatua kadhaa, ikiwamo kulipa madeni ya Serikali yaliyolimbikizwa, urasimishaji wa nguvu kazi, ukarabati wa vifaa vya uzalishaji ili kuigeuza TMCL kutoka machinjio pekee hadi usindikaji kamili wa nyama. Kukidhi malengo hayo, Bodi ilipendekeza kwa Wanahisa wa TMCL, ambao waliridhia, uteuzi wa Msimamizi Mtawala (Administrative Receiver) atathmini hali ya TMCL na kupendekeza namna ya kuimarisha zaidi na kuweka mkakati wa kuipa uwezo wa muda mrefu. Taarifa yake kwa Wanahisa iliidhinishwa kwa utekelezaji katika kikao chao maalum tarehe 27 Novemba 2019. Taarifa ya Administrative Receiver vilevile iliwasilishwa Wizarani, na Mheshimiwa Waziri mwenyewe aliomba na kupewa taarifa hiyo tarehe 27 Desemba 2019.

Izingatiwe kwamba ni Bodi halali ya TMCL ndiyo ilifanikisha utayarishaji wa taarifa za kifedha zilizolimbikizwa kinyume na sheria kwa kipindi cha miaka sita (6), kati ya mwaka 2009 na 2015, na kukaguliwa na wakaguzi huru wa nje wanaotambulika. Taarifa za mahesabu hayo hazioneshi uwepo deni lolote kwa kiwango kilichotajwa katika taarifa zinazosemekana kutolewa na Waziri kwenye vyombo vya habari. Hivyo basi chanzo cha deni cha Shilingi bilioni 15, ambalo NICOL inatuhumiwa nalo, ni kitendawili, na hasa inapobainika kwamba mwanahisa mwenza (Wizara) iliwahi kushiriki kuzuia utayarishwaji na ukaguzi wa mahesabu ya kampuni kwa miaka 6.

Kwa hiyo, mbali na kutokuwepo na chanzo chochote au uhalali wa deni kama NICOL ilituhumiwa nalo, ni dhahiri kwamba kwa vyovyote vile NICOL haiwezi kuwa inadaiwa shilingi bilioni 9.7 na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mwanahisa mwenza), au shilingi bilioni 5.4 na TMCL (kampuni tanzu iliyokuwa ikipewa mikopo nafuu na NICOL), kwani NICOL haihusiki kwa vyovyote vile na masuala ya uendeleshaji wa TMCL, ambayo ni kampuni inayojitegemea kisheria.

Pamoja na kwamba mpaka sasa NICOL haijapokea rasmi shutuma na madai kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, NICOL inakanusha bila kusita madai yote kwa ujumla wake yanayosemekana yalitolewa na Wizara hiyo katika vyombo vya habari. Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia Wanahisa kuwa NICOL itaendelea kushirikiana na Serikali kwa karibu katika kutekeleza majukumu yake yote, na kuzingatia sheria, sera za nchi na utawala bora, na itafanya yote yanayowezekana kulinda masilahi yao.

KWA AMRI YA BODI

NICOL

Close

Dodoso Kampuni Tanzu NICOL

Close

NICOL Subsidiary Information

Funga

Dodoso Uwekezaji soko la hisa DSE

Close

Investment in DSE Listed company Profile

X Funga

Dodoso Uwekezaji

X Close

Investment Profile

Close

X Funga

Taarifa(Tangazo)

X Close

Announcement of

Funga

Wasifu kwa ufupi

Close

Bio Profile

Close

Close
>
Close

Close
>
Close

>